Jumatano , 31st Jul , 2019

Wakazi wa Kata za Shanwe, Mkanyagio na Misunkumilo Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi wamelalamikia uwepo wa wanyama Waharibifu aina ya Kiboko, ambao wamekuwa wakihatarisha maisha yao na kuharibu mazao.

Kwa mujibu wa wakazi hao, viboko wamekuwa wakitoka katika bwawa la Milala, ambalo lilikuwa chanzo cha maji, na sasa limekuwa hifadhi ya wanyama hao ambao wanatoka bwawani na kwenda katika makazi ya watu.

Wakieleza kwa masikitiko makubwa, baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Mpanda wameeleza kukerwa na wanyama hao na kuomba mamlaka husika kuchukua hatua au kuwaruhusu ili wawauwe.

Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Mhe Sebastian Kapufi, akiiongea na Wananchi hao katika mkutano wa hadhara amebainisha kuwa tayari tatizo hilo ameshaliwasilisha Bungeni na Waziri wa Maliasili ameahidi kulifanyia kazi.

Bwawa la Milala lilichimbwa miaka ya 1956 kwa ajili ya chanzo cha Maji kwa Wakazi wa Manispaa ya Mpanda lakini sasa imekuwa kama hifadhi ya wanyama aina ya Boko ambao ni zaidi ya 50 wanaoishi katika bwawa hilo.