Jumapili , 14th Dec , 2014

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini Tanzania umefanyika leo huku ukikabiliwa na kasoro kadhaa katika maeneo tofauti ya nchi na hata kupelekea katika baadhi ya mitaa uchaguzi kutofanyika kabisa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Jumanne Sagini akizungumza na vyombo vya habari jana kuhusiana na uchaguzi huo. Sagini aliwahakikishia Watanzania kuwa maandalalizi kwa ajili ya uchaguzi wa leo yamekamilika.

Jijini Dar es Salaam, EATV imefika katika mitaa kadhaa ambapo mtaa wa Sinza A, Kata ya Sinza A, kulikuwa na changamoto ya kutokuwepo kwa wino jambo ambalo lingeweza kutoa mwanya kwa mtu kuweza kurejea kupiga kura zaidi ya mara moja.

Hali ilikuwa mbaya katika mtaa wa Kazima uliopo Kinondoni, baada ya uchaguzi kushindwa kufanyika kabisa, kufuatia vurugu zilizosababisha msimamizi wa uchaguzi katika kituo hicho kuahirisha uchaguzi huo.

Katika kituo hicho, watu watatu wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano kutokana na kuhusika kwao na vurugu hizo, kwa mujibu taarifa zilizothibitishwa na mkuu wa polisi mkoa wa Kinondoni Kamanda Camilius Wambura.

Aidha katika kituo cha Ilala Shariff Shamba, uchaguzi umelazimika kuahirishwa hadi Jumapili ijayo kutokana na kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura, huku hali ikiwa tofauti katika kituo cha Kata ya Kariakoo ambapo wazee na walemavu walilalamikia kutopewa kipaumbele kupiga kura kama taratibu zinavyoagiza.