Jumamosi , 16th Oct , 2021

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amewataka wote wanaofanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa kutumia siku tatu zilizosalia kuhama ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla

Hata hivyo RC Makalla amemuelekeza mkuu wa wilaya ya Ilala, kuhakikisha wafanyabiashara wote waliopanga meza katikati ya barabara za mitaa, Kariakoo na Msimbazi kuondolewa ili barabara zibaki wazi kwa ajili ya magari kushusha mizigo.

RC Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya kuwapanga machinga kwa kila wilaya ambapo amesema kwa hizi siku tatu serikali itaongeza nguvu kwenye kutoa matangazo na elimu ili kuhakikisha ifikapo Oktoba 18, 2021, kila mfanyabiashara awe kwenye eneo alilopangiwa.

RC Makalla pia ameelekeza maeneo yote watakayopelekwa wafanyabiashara ikiwemo masoko, daladala zishushe abiria kwenye maeneo hayo ili kuchochea biashara.

Miongoni mwa wafanyabiashara wanaotakiwa kupangwa ni wale waliojenga vibanda juu ya mitaro na mifereji, wanaofanya biashara kwenye maeneo ya watembea kwa miguu, wanaofanya biashara kwenye hifadhi ya barabara, wanaofanya biashara mbele ya maduka, na wanaofanya biashara kwenye taasisi za umma zikiwemo shule.