Jumanne , 8th Aug , 2023

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, amewataka wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na kanuni  zake, maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume ili kuwa na uchaguzi wa huru na wa haki.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele

Jaji Mwambegele ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo kwa Wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi leo Agosti 8, 2023 mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na Kata sita za Tanzania Bara utakaofanyika Septemba 19, 2023.

Uchaguzi katika jimbo la Mbarali unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Francis Mtega, kilichotokea Julai Mosi, 2023, baada ya kugongwa na Trekta.

Uchaguzi huo utafanyika katika Jimbo la Mbarali na kata zitakazofanya uchaguzi huo ni Kata ya Nala iliyopo halmashauri ya Jiji la Dodoma, Kata ya Mfaranyaki iliyopo halmashauri ya Manispaa ya Songea, Kata ya Mwaniko iliyopo halmashauri ya wilaya ya Misungwi, Kata ya Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Rombo, Kata ya Mtyangimbole iliyopo halmashauri ya wilaya ya Madaba na Kata ya Old Moshi Magharibi iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Moshi.