
Taarifa ya kufungwa kwa kanisa hilo imetolewa na Makamu wa Askofu wa Jimbo hilo Padri Ovan Mwenge Septemba 01, 2023 ambapo taarifa inaeleza kuwa usiku wa kuamkia Septemba 01, 2023, watu wasio julikana walivunja ukuta wa kanisa na kuingia ndani na kuvunja kifaa cha kuhifadhia sakramenti takatifu (Tabernakulo).
“Kwa kadri ya maelekezo na sheria ya kanisa kaanuni ya 1211-1213 na kwa maelezo ya Askofu Severine Niwemugizi kanisa hilo litafungwa kwa siku 30 kuanzia septemba mosi na baada ya maboresho na ukarabati mdogo wa kanisa hilo litabarikiwa na kutakaswa ili liendelee kutumika” imesema taarifa hiyo
Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa kwa kipindi hicho waumini wa jimbo hilo wamehimizwa kusali na kufunga pamoja na kufanya toba ya malipizi kwa mwenyezi mungu ili abadilishe mioyo ya watu wenye nia ovu kwa mambo matakatifu.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Geita RPC Safia Jongo Kwa njia ya simu wakati akizungumza na EATV amesema bado hajapata taarifa hiyo.
Hili linakuwa tukio la pili kutokea mkoani Geita ambapo mwezi februari ,2023 kijana mmoja mkazi wa Geita alivamia na kufanya uharibifu wa vifaa vya Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Geita vyenye thamani ya TZS. Million 48.2