Jumapili , 1st Mar , 2020

Kampuni ya BM Motors iliyopo eneo la Zegereni katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani, imeingia kwenye orodha ya kampuni zinazounda na kutengeneza mabasi ya abiria nchini Tanzania.

Moja ya basi lililoundwa na kampuni hiyo

Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bw. Jonas Nyagawa amesema kuwa kampuni inatengeneza mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 45 hadi 57, huku wakiwa na msukumo wa kuunga mkono sera ya viwanda nchini.

Serikali imekuwa ikisisitiza uanzishaji wa viwanda ili nchi yetu ifikie uchumi wa kati na Wananchi waweze kuwa na kipato cha kati, ili kufikia azma hiyo lazima kujengwe viwanda vingi na wananchi nao wapate ajira”, amesema Nyagawa.

Bwana Nyagawa amesema vifaa vinavyotumika kuunda mabasi hayo vinatoka sehemu mbalimbali, huku asilimia 55 vikitoka nje ya nchi, ambapo tangu karakana hiyo ianze kufanya kazi tayari mabasi mawili yameshaundwa na yako katika hatua za mwisho za usajili ili kuanza kufanya kazi.

Kila kitu kinawezekana, Watanzania wanapaswa kuwa na uthubutu. Karakana hii inaunda mabasi na sio kwamba vifaa vyote vinatoka nje ya nchi, vingine vinapatikana hapa hapa nchini”, amesema.

Kufuatia uanzishwaji wa kampuni hiyo, hadi sasa imetoa ajira kwa Watanzania 15 huku baadhi yao wakiongeza ujuzi kutoka kwa Wataalamu wa nje ya nchi wanaofanya kazi na kampuni hiyo.

Fundi Mkuu wa Kampuni hiyo, Frank Ngewe amezungumzia fursa aliyoipata katika kampuni, “kwanza tunamshukuru Rais wetu na Serikali kwa ujumla kwa kukazania Sera ya Tanzania ya Viwanda. Watanzania wengi hususani vijana hivi sasa wanapata ajira na kujikwamua kimaisha kutokana na kuanzishwa kwa viwanda nchini”, amesema.