Alhamisi , 5th Oct , 2023

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, ameahidi kujenga kisima kikubwa cha maji katika shule ya sekondari Kibacha wilayani Same, kwa lengo la kuendeleza kilimo cha mbogamboga na kuboresha lishe bora shuleni hapo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki

Ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2023 katika mahafali ya 7 ya Kidato cha Nne  katika  Shule ya sekondari Kibacha, wilayani Same mkoani Kilimanjaro. 

 "Nimeguswa na ujumbe wa igizo la watoto hawa kuhusu changamoto ya maji, naomba nitamke kuwa nitaijengea shule hii kisima kikubwa cha maji ambacho pia kitawezesha kuendeleza kilimo cha mbogamboga na viazi lishe kwa ajili ya kuchangia lishe ya watoto wetu na hivyo kutimiza azma ya serikali ya kuhakikisha suala la lishe shuleni linapewa kipaumbele," amesema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki amefafanua kuwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na ilishaiona changamoto ya maji wilayani hapo hivyo, ipo kwenye hatua nzuri ya ukamilishwaji hadi kufikia mwaka 2024 Wilaya ya Same itakuwa na maji ya kutosha.

Katika hatua nyingine amewaasa vijana wanaohitimu kidato cha nne kuzingatia maadili ya  Mtanzania na kuzingatia masomo.