Jukwaa la Katiba nchini Tanzania (JUKATA) limeitaka serikali kutangaza kuanza kwa mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya kwani mchakato huo haukufika mwisho.
Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bw. Deus Kibamba amesema kuwa mchakato huo haukuwa na maridhiano baina ya wajumbe hali iliyopelekea baadhi ya wajumbe kujitoa kwenye mchakato huo..
Kwa upande mwingine Kibamba ameitaka serikali kupeleka muswada bungeni ili kuwezesha mchakato wa Katiba mpya kuanza mara moja kwa manufaa ya nchi.
Aidha jukwaa halijaridhishwa na kitendo cha wabunge wa upinzani kutoka nje ya bunge kwa kipindi kirefu kwani hali hiyo inapelekea baadhi ya maamuzi kufanyika bila ya wabunge kutimia akitolea mfano bajeti ya serikali imepitishwa na wabunge 85 pekee kati ya wabunge zaidi ya 400 waliokusudiwa.






