Ijumaa , 12th Sep , 2014

Jukwaa la Katiba nchini Tanzania limeonya kuwa litahamisha maandamano ya wananchi kutoka sehemu mbali mbali nchini, kwenda kufunga ofisi za Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba.

Hatua hiyo itafikiwa iwapo mwenyekiti wake Mh. Samuel Sitta hatasitisha vikao vya bunge hilo mara moja kutokana na kutokuwa na umuhimu kwa nchi hasa baada ya kufikiwa kwa muafaka baina ya vyama vikuu vya upinzania kwenye bunge la katiba.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bw. Deus Kibamba amesema hatua ya kutaka kufunga ofisi za Bunge Maalumu la Katiba inatokana na kile alichoeleza kuwa matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi zinazotumika kwa matumizi yasiyo na tija.

Kwa mujibu wa Kibamba, kuendelea kwa bunge hilo hakuna mantiki yoyote hivi sasa ambapo pia Jukwaa limependekeza Sitta pamoja na mwanasheria Mkuu wa Serikali jaji Frederick Werema wasiruhusiwe kugombea nafasi yoyote ya kisiasa kwa kipindi cha miaka kumi kutokana na kile ilichodai kuwa ni kuhusika kwao katika kuvuruga mchakato wa katiba.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mhe. Samwel Sitta amelitupia vijembe kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kusema kuwa wajipange mwakani watakapo shindwa vibaya katika uchaguzi mkuu kurejea katika fani ya uigizaji waliyoizoea.

Mhe. Sitta amesema kuwa kundi la Ukawa limekuwa likipotosha kila jambo na hata juzi walipokua wamekutana na Rais Jakaya Kikwete wakakubaliana mambo muhimu walipotoka hapo wakageuka na kuja na mambo mengine kabisa.

Mh, Sitta amesema kuwa jambo ambalo wanafanya wanasiasa hao ni kama wasanii wa maigizo kwa kuwa walishafikia makubaliano na Rais kuhusu kuendelea kwa bunge hilo mpaka pale litakapopata Rasimu ya Katiba itakayo pendekezwa.