Alhamisi , 22nd Oct , 2020

Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Dkt John Magufuli, amemuahidi aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki kupitia, CHADEMA, Joshua Nassari, ambaye kwa sasa yupo CCM kuwa atampa kazi kwa sababu ni kijana anayejitambua.

Kushoto ni mgombea urais kupitia CCM Dkt John Magufuli na kulia ni Joshua Nassari.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 22, 2020, wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika, Arumeru mkoani Arusha, na ndipo alipomkaribia Nassari kwa ajili ya kuwaombea kura wagombea ubunge wa jimbo hilo.

"Ninamshukuru sana kijana Nassari ni kijana anayejitambua, ebu mpe 'Mic' asalimu hapa na aombe kura kwa ajili ya wabunge wengine, huyu anajitambua alijua alikuwa amekosea na mimi Nassari nakuambia nitakupa kazi, ebu omba kura kwa ajili ya waheshimiwa hawa", amesema Dkt Magufuli.

Kwa upande wake Joshua Nassari akatumia nafasi hiyo kumuomba msamaha Dkt Magufuli, "Mh. Rais mtu anayeomba radhi ni anayefahamu tendo la ujasiri na mimi naomba leo niuvae ujasiri nije mbele yako na wana Meru kama kuna mahali nimewahi kukosea ninakuomba unisamehe, ninaomba radhi kwa niaba ya watu wa Meru, mwaka 2015 katika uwanja huu niliwaomba watu hawa wapeleke kura mahali pengine".