Alhamisi , 15th Aug , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, leo Agosti 15 amekutana na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini Cyril Ramaphosa, Ikulu ya Dar es Salaam na kufanya mazungumzo ya faragha na kwa pamoja wameweka makubaliano yatakayoleta tija kiuchumi.

Katika hotuba yake Rais Magufuli amesema,  mazungumzo yake na mgeni wake yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, ukizingatia nchi ya Afrika Kusini ni nchi yenye uchumi mkubwa barani afrika kwa kushika nafasi ya pili baada ya Nigeria, na kujadili namna ambavyo mataifa hayo yataweza kuimarisha biashara na uwekezaji.

''Tanzania na Afrika ya Kusini ni  washirika wakuu wa biashara tunaongoza kwa kuongoza kufanyabiashara ndani ya jumuiya ya nchi za SADC, Mwaka 2018 thamani ya biashara kati yetu  ilifikia dolla bilioni 1.8 kutoka dolla bilioni 1.1 mwaka  2017,  na sisi Tanzania  tuliuza Afrika Kusini bidhaa zenye thamani ya shilingi dolla milioni 743.02 ambayo ni sawa na asilimia 70 ya mazao yetu kwenye  nchi za SADC sawa na asilimia 16.7 ya mazao yetu yote nje ya nchi'', amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amewakaribisha wafanyabiashara wa Afrika ya Kusini, kuja kuwekeza nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kukuza sekta ya viwanda, afya , kilimo na uvuvi pamoja na usindikaji wa mazao mbalimbali.