Jumatatu , 5th Mei , 2014

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, ameahidi kuwa katika siku za karibuni, anatarajia kuteua majaji wa mahakama kuu na wa mahakama ya rufaa 20, hatua ambayo amesema inalenga kuharakisha usikilizaji wa kesi na mashauri katika mahakama hizo.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya majaji wa mahakama kuu na mahakama ya rufaa nchini.

Aidha amesema pia serikali ipo katika mchakato wa ujenzi wa majengo ya mahakama kuu katika mikoa minne nchini, katika hatua alizosema pia zinalenga kuboresha utendaji wa idara ya mahakama.

Rais Kikwete ametoa ahadi hizo leo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 12 wa kimataifa wa chama cha majaji wanawake duniani, mkutano unaofanyika jijini Arusha.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, rais Kikwete amewataka washiriki wa mkutano huo watumie majadiliano yao katika kuboresha shughuli za mahakama katika nchi zao, ili ziweze kutoa haki sawa kwa makundi yote pasipo ubaguzi.

Amesisitiza umuhimu wa kuboresha utendaji wa mahakama katika nchi zao kutokana na ukweli kwamba sheria zinazotumika katika nchi nyingi hivi sasa ni zile zilizoachwa na wakaloni ambazo kimsingi zimepitwa na wakati.