Jumanne , 28th Apr , 2015

Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ikiwa ni pamoja na kutumia utashi wao kufanya maamuzi yaliyo sahihi na kumchagua kiongozi atakayeweza kuleta mabadiliko ya nchi.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Ummy Mwalimu akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Ummy Mwalimu wakati akizungumza na wakazi wa jiji la Tanga ambapo amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kusikiliza sera za kila chama na kila mgombea.

Sanjari na hayo amewataka wananchi kujitokeza kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kuielewa pamoja na kufanya maamuzi ya kuipigia kura ya maoni baada ya kuisoma na kuielewa katiba hiyo.

Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais unatarajiwa kufanyika mwezi Oktober mwaka huu, hivyo wananchi wanatakiwa kuwachagua viongozi watakaojua msimamo wa Tanzania, watakaopigania haki, usawa na demokrasia ya kupendwa na watu wengi kuliko wachache.