Jumanne , 7th Mei , 2024

Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha limesema litaendelea kuwashukuru wananchi wanaoendelea kushiriki katika jitihada za serikali katika kuboresha mazingira bora na ya kisasa katika vituo vya Polisi mkoani humo huku likibainisha kuwa litaendelea kutoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Polisi Jamii mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Peter Lusesa, wakati akikabidhiwa ofisi ya Upelelezi wilaya baada ya kufanyiwa marekebisho na wadau wa masuala ya usalama ili kutoa huduma bora kwa wateja.
 
ACP Lusesa amesema jeshi hilo kwa sasa nalo limebadilika kiutendaji kutokana na mabadiliko ya kidunia ambapo amewaomba wananchi hao waliojitolea kuboresha ofisi hiyo, watambue kuwa Jeshi hilo litaendelea kutoa huduma bora na za kisasa zinazoendana na mabadiliko ya dunia ya leo.
 
Sambamba na hilo ACP Lusesa amewataka Maafisa, wakaguzi na askari wanaotoa huduma katika kituo hicho kuhakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wananchi ambao wanalitegemea Jeshi la Polisi huku akiwataka kutambua kuwa Mkoa wa Arusha ndio kioo cha Tanzania katika anga la kimataifa na kitovu cha utali hapa nchini.