Jumamosi , 18th Apr , 2026

Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi imemhukumu Sweetbert Lyankuba (41) mkazi wa Mamba kutumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na nyara za serikali nyama ya mnyamapori Nguruwe kiasi cha kilogramu 420.

Hukumu hiyo imetolewa April 16, 2026 na hakimu wa mahakama hiyo Mhe. Andrew Njau ambapo amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akikabiliwa na shitaka la kupatikana na nyara za serikali ambazo alikamatwa nazo akiwa amebeba kwenye baiskeli huko eneo la Kiwanjani katika Hifadhi ya Taifa Katavi.

Mhe. Njau amesema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha sheria ya uhifadhi wa wanyamapori kifungu namba 86 (1) (2) (c) (3) ikisomwa pamoja na sheria ya makosa ya uhujumu uchumi kifungu namba 57 (1) 61 (2).

Akisoma hukumu hiyo Mhe. Njau alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Oktoba 23, 2025 na kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 14, 2025, ambapo ameongeza kuwa mahakama imejiridhisha na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo bila shaka na mtuhumiwa kutiwa hatia kwa kosa hilo.

Mshtakiwa huyo licha ya kuomba mahakama hiyo imuonee huruma na kumpunguzia adhabu, mahakama ilitupilia mbali ombi lake na kusema imetoa hukumu hiyo kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.   

Katika hatua nyingine hiyo imemuhukumu Andrea Shauritanga (36) mkazi wa Utende kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kupatikana na madawa ya kulevya (Bangi) kete 76 na Gramu 73.4. 

Hukumu hiyo imetolewa April 17, 2026 na hakimu wa mahakama hiyo Mhe. Andrew Njau ambapo amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akikabiliwa na shitaka la kupatikana na madawa ya kulevya ambayo alikamatwa nayo akiwa ameyahifadhi katika nyumba anayoishi kwa lengo la kujipatia kipato. 

Akisoma hukumu hiyo Mhe. Njau alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Februari 02, 2026 na kufikishwa mahakamani April 16, 2026 ambapo ameongeza kuwa Mtuhumiwa amekiri kutenda kosa hilo na mahakama imejiridhisha pasi na shaka mtuhumiwa kutiwa hatiani kwa kosa hilo kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 11 (1) d ya mwaka 2023.  

Mshtakiwa huyo licha ya kuomba mahakama hiyo imuonee huruma na kumpunguzia adhabu, mahakama ilitupilia mbali ombi lake na kusema imetoa hukumu hiyo kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.