Ijumaa , 15th Sep , 2023

Katika kuhakikisha jamii inajenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya CCBRT leo wameendesha zoezi la kupima afya na kutoa elimu ya kukabiliana na maradhi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dkt. Gaspa Shayo, elimu iliyotolewa ni pamoja na namna ya kukabiliana na maradhi ya Tezi Dume, kufanya uchunguzi wa maradhi ya macho pamoja na saratani ya matiti.

Amesema kuwa, uchunguzi huo ni hatua ya awali na kwamba, mtu akibainika kuwa na tatizo, atatakiwa kufika Msasani ilipo hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu.

"Hili ni zoezi endelevu na kwa kweli litawasaidia watu kujua afya zao kwani ni muhimu sana kujenga utamaduni wa kujua afya yako" amesema Dkt. Gaspa

Kwa upande wake Diana Mtovu na Winnie Laurance ambao wamepata huduma katika zoezi hilo wamesema ni jambo jema kwa hospitali hiyo kudhamiria kujenga utamaduni kwa Watanzania kupenda kujua afya zao mapema.

Kwa sasa CCBRT imeendelea kutanua huduma zake ikiwemo kuwa na huduma ya mama na mtoto na huduma kwa wasojiweza.