
Jaji Frank Caprio ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 88 kutokana na kusumbuliwa na kansa ya Kongosho ( Pacreatic Cancer) kwa muda. Kifo chake kimetangazwa kwenye ukurasa wake wa Instagram jana Jumatano, Agosti 20, 2025 na mtoto wake David Caprio.
Caprio alikuwa jaji na mwanasiasa wa Marekani ambaye aliwahi kuwa jaji mkuu wa mahakama ya manispaa ya Providence, Rhode Island, na mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Rhode Island kwa Elimu ya Juu.
Wengi wanamkumbuka Jaji Frank Caprio kama mtu mwenye huruma nyingi alipokuwa kwenye chumba cha mahakama. Uchangamfu, ucheshi, na fadhili zake ziliacha kivutio cha kudumu kwa kila mtu ambaye alikuwa na pendeleo la kumjua au kusikia maneno yake.
Jaji Caprio alikuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii ambako klipu za video zake akiwa mahakamani zimekuwa zikisambaa. Video hizo zinaonyesha huruma yake katika chumba cha mahakama hasa kwa wale wakosaji ambao simulizi zao zilikuwa zinatia huruma. Ameacha mke, watoto 5, wajukuu 7 na vitukuu wawili.