Jumapili , 25th Aug , 2024

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imesema kujiandikisha kuwa mpiga kura zaidi ya mara moja ni kosa la kisheria kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 114(1) cha sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024.

Jaji Asina Omari, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Jaji wa Mahakamu Kuu

Hayo yamesemwa na Jaji Asina Omari, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Jaji wa Mahakamu Kuu wakati akifungua mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi mkoani Manyara leo tarehe 25 Agosti, 2024.

"Nitoe rai kwenu, muwaelimishe wananchi wanaokwenda vituoni kwa ajili ya kuomba kuandikishwa kuwa wapiga kura, kuomba kuandikishwa kuwa wapiga kura ni mara moja tu ili kuepuka uvunjaji wa sheria,"amesema Jaji Asina.

Mjumbe wa Tume, Mhe.Jaji Asina Omari amewapongeza wadau wa uchaguzi na wananchi wa Manyara kwa kupata fursa ya mkoa wao kuwa katika mzunguko wa nne wa uboreshaji wa daftari na kuwataka wawe mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa ili zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi na mafanikio makubwa.