Jumamosi , 15th Mei , 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo ametoa siku kumi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma kuhakikisha anasajili mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa ili uweze kupata cheti cha tathmini ya mazingira.

Jengo la Machinjio ya Kisasa la Manispaa ya Kigoma ambalo ujenzi wake haujafuata taratibu.

Mhe. Jafo amesema hayo akiwa kwenye ziara yake mkoani Kigoma alipotembelea machinjio ya Manispaa hiyo, ambapo amesema endapo Manispaa itashindwa kusajili mradi huo wa machinjio ya kisasa kwa kipindi tajwa atasitisha ujenzi huo.

"Naagiza mradi huu usajiliwe mapema iwezekanavyo, na lengo la kufanya hivi si kupata cheti tu bali muhimu ni kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala muhimu ya kuzingatia katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira,” amesema Mhe. Jafo.

Waziri Jafo aliongeza, “Hivi sasa kuna mfumo wa kusajili miradi kwa njia ya mtandao na miradi yote naiona hapa kwenye tablet yangu sasa ikifika tarehe 25/05/2021 sijaona mradi wenu nitasitisha ujenzi wenu,"

Sambamba na hilo Mhe. Jafo amewataka wawekezaji kote nchini kusajili miradi yao ili iweze kukidhi vigezo vya kupatiwa cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira kinacho ainisha namna bora ya kupunguza madhara ya kimazingira yatokanayo na utekelezaji wa miradi.