Ijumaa , 18th Mar , 2016

Serikali ya India imetangaza neema kwa wafanyabiashara wa Tanzania wanaotaka kufanya biashara nchini humo ambao watanufaika na fursa ya kusafiri bila ya kulazimika kuwa na visa kama ilivyo kwa mataifa mengine.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Mkoani Mbeya Bw. Lwitiko Mwakaluka

Balozi wa India Nchini Sandeep Arya amesema hayo Jijini Mbeya mara baada ya kuhudhuria mkutano wa baraza la biashara lililoandaliwa na chama cha wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo nchini (TCCIA).

Balozi huyo wa India amesema kuwa kwa sasa mfanyabiashara au mtanzania halazimiki kufika hadi jijini Dar es salaam kwa ajili ya visa bali atajaza fomu maalum kupitia tovuti ya ubalozi wa India nchini.

Sandeep amesema sasa wafanyabiashara wa kitanzania watalazimika kulipa dola moja na nusu sawa na shilingi 3,273 za kitanzania ambapo hapo awali walikuwa wanalipa dola 50 kwa ajili ya visa ya kusafiria kwenda nchini India.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Mkoani Mbeya Bw. Lwitiko Mwakaluka amesema kuwa watatumia vyema fursa hiyo kwa manufaa yao na watanzania kwa ujumla sasa wanaandaa mkutano mwingine kwa ajili ya mipango ya kuboresha biashara kati ya India na Tanzania.