Jumamosi , 19th Mei , 2018

Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imewathibitishia wapenda soka na wananchini wa kiujumla kuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli atashiriki kikamilifu katika zoezi la kupokea Kombe la Ubingwa wa CECAFA pamoja na kuwakabidhi kombe la mabingwa wa michuano ya ligi kuu.

Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa asubuhi ya leo Mei 19, 2018 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais- Ikulu, Gerson Msigwa kupitia ukurasa wake maalum wa twitter na kusema Rais Dkt. Magufuli ataungana na wanamichezo katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

"Mhe. Rais  Magufuli leo ataungana na wanamichezo kupokea kombe la ubingwa wa CECAFA kutoka timu ya Serengeti Boys, kuipokea timu ya TSC iliyoibuka mabingwa wa pili wa dunia huko Urusi na kukabidhi kombe kwa Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kuanzia saa 8 mchana", imesema taarifa ya Msigwa.

Tukio hili la kimichezo ni kwa Rais Dkt. Magufuli ndio la kwanza kulifanya tokea alipoingia madarakani na hivyo atakuwa amewawekea historia kubwa klabu ya Simba SC kukabidhiwa kikombe na Rais pamoja na Serengeti Boys.