Jumapili , 19th Oct , 2025

"Mhe. John Wegesa Heche ameondoka nchini na kuvuka mpaka na kuingia nchi Jirani bila kufuata taratibu na Kanuni za Uhamiaji zilizoundwa chini ya Sheria ya Uhamiaji sura ya 54"

Idara ya Uhamiaji nchini imesema kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Bara, John Wegesa Heche ameondoka nchini Tanzania na kuingia nchi Jirani bila kufuata utaratibu kupitia Kituo cha Uhamiaji cha Sirari mkoani Mara.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Idara hiyo SSI Paul Mselle jana imeeleza kuwa Heche alivuka mpaka jana Oktoba 18 bila kufuata utaratibu na Kanuni za Uhamiaji zilizoundwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54.

“Leo tarehe 18 Oktoba, 2025 katika Kituo cha Uhamiaji cha Mpaka wa Sirari mkoani Mara, Mhe. John Wegesa Heche ameondoka nchini na kuvuka mpaka na kuingia nchi Jirani bila kufuata taratibu na Kanuni za Uhamiaji zilizoundwa chini ya Sheria ya Uhamiaji sura ya 54”, taarifa hiyo imesema.

Kufuatia tukio hilo, idara hiyo imetoa wito kwa raia wa Tanzania na wageni wote wanaotoka na kuingia nchini kufuata taratibu na kanuni zinazoongoza uingiaji, ukaazi na utokaji wa watu nchini ili kuepuka kutenda kosa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Taarifa hii imekuja ikiwa siku ya jana kulikuwa na taarifa nyingi kutoka kwa Heche mwenyewe akidai kuzuiwa kuvuka mpaka kwenda nchini Kenya kwa ajili ya kumzika aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, huku hati yake ya kusafiria alinyang'anywa

Kupitia taarifa maalum ya chama chake cha CHADEMA iliyotoka Oktoba 17, 2025 ilieleza kuwa Heche na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho watasafiri kwenda Bondo nchini Kenya kushiriki mazishi ya Odinga baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu kuwaagiza viongozi hao kwenda kumzika Odinga.