Alhamisi , 15th Oct , 2015

Wakati kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein akisema watu wenye ulemavu wa ngozi, wana haki ya kuishi huru bila ubaguzi na hofu yoyote, Tanzania imesema inaendelea kuchukua hatua kutokomeza mauaji ya albino.

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa mkutano wa Umoja huo

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi amekiri kuwa mauaji ya albino nchini ni janga lakini serikali imechukua hatua watu wengine wamefungwa kwa kutiwa hatiani na wengine wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.

Akigusia filamu iitwayo The Boy from Geita itakayooneshwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa leo, Balozi Manongi amesema filamu hiyo ina maudhui yanayoonesha kuwa serikali haijachukua hatua zozote za kupiga suala hilo.

Alipozungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Balozi Manongi amesema janga la mauaji ya albino ni la kila mtu uwe Umoja wa Mataifa, serikali ya Tanzania na hata mashirika yasiyo ya kiserikali yanayopigania maslahi ya kundi hilo hivyo ubia wa dhati ni muhimu badala ya kunyoosheana vidole.