Jumanne , 24th Sep , 2019

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, amelipongeza jeshi lake kwa namna ambavyo limeweza kupambana na kukomesha mauaji ya raia yaliyokuwa yakifanyika Wilayani Kibiti mkoani Pwani.

IGP Sirro ameyabainisha hayo leo Septemba 24, 2019 Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao chake na maafisa wandamizi pamoja na makamanda wa mikoa na vikosi mbalimbali na kueleza kuwa suala la mauaji ya Kibiti liliwapa changamoto kubwa pengine bila ushirikiano wao wasingeweza.

''Habari ya Kibiti ndani ya Jeshi la polisi haitofutika, issue ilikuwa ni kubwa sana kwa challenge jeshi la polisi,  lakini slogan yetu ya umoja ndiyo nguvu yetu ndio imetufikisha hapa tulipo. Sasa hivi ukizungumzia Kibiti hata viwanja vimepanda bei, wanasiasa wanafanya siasa zao ni heshima ya jeshi lakini pia ni heshima kwa vyombo vingine vya ulinzi na usalama'', amesema IGP Sirro.

Aidha IGP Sirro amewataka maafisa waandamizi wa jeshi hilo kufanya kazi kwa weledi pamoja na kusimamia sheria ikiwemo kuongeza mikakati ya kupunguza matumizi ya silaha na uhalifu.