
Israel na kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas wametia saini makubaliano siku ya ya leo Alhamisi Oktoba 9, ili kusitisha mapigano na kuwaachia huru mateka wa Israel badala ya wafungwa wa Kipalestina, ikiwa ni awamu ya kwanza ya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump kumaliza vita huko Gaza.
Waisraeli na Wapalestina kwa pamoja wamefurahi baada ya makubaliano hayo kutangazwa, ikiwa ni hatua kubwa zaidi kuwahi kuchukuliwa kumaliza miaka miwili ya vita ilyopelekea zaidi ya Wapalestina 67,000 kuuawa, na yanalenga kuwarudisha mateka wa mwisho waliotekwa na Hamas katika mashambulizi yaliyoianzisha.
Maafisa wa pande zote mbili wamethibitisha kusaini makubaliano hayo kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja katika eneo la mapumziko la ufukwe la Sharm el-Sheikh nchini Misri.
Chini ya makubaliano hayo mapigano yatakoma, Israel itajiondoa kwa sehemu kutoka Gaza na Hamas itawaachilia mateka wote waliosalia iliowakamata katika shambulio lililochochea vita la Oktoba 7, 2023, badala ya mamia ya wafungwa wanaoshikiliwa na Israel.
Makundi ya malori yaliyobeba chakula na misaada ya kimatibabu yataruhusiwa kuingia Gaza ili kuwaokoa raia, mamia kwa maelfu wakiwa wamejificha kwenye mahema baada ya wanajeshi wa Israel kuharibu nyumba zao.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema usitishaji huo wa mapigano utaanza kutekelezwa mara tu makubaliano hayo yatakapoidhinishwa na serikali yake, ambayo yataitishwa baada ya kikao cha baraza la mawaziri la usalama baadaye leo Alhamisi.
Wakati wengi wa Wapalestina katika ukanda wa Gaza wakifurahia uamuzi huo bado kuna wasiwasi. Hata baada ya mkataba huo kutiwa saini, chanzo kimoja cha Wapalestina kimesema orodha ya Wapalestina watakaoachiliwa bado haijakamilika. Kundi hilo linatafuta uhuru kwa baadhi ya wafungwa mashuhuri wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel pamoja na mamia ya watu waliozuiliwa wakati wa shambulio la Israel.
Hatua zaidi katika mpango wa Trump wenye vipengele 20 bado hazijajadiliwa na pande zote ikiwemo jinsi gani Ukanda wa Gaza uliosambaratishwa utakavyotawaliwa pindi mapigano yatakapomalizika, na hatima ya mwisho ya Hamas, ambayo hadi sasa imekataa matakwa ya Israel ya kuipokonya silaha.