Jumatatu , 14th Apr , 2014

Watu 17 waliojeruhiwa kwenye mapaja na miguuni na bomu lililorushwa kwenye baa ya Night Park mkoani Arusha jana wamelazwa katika hospitali ya mkoa Maunt Meru, huku mmoja akiwa amelazwa hospitali inayomilikiwa na kanisa la KKKT ya Selian.

Picha ya moja ya mabomu ya mkono ambayo mara nyingi hutumika kwa kurushwa kwa lengo la kudhuru au kujeruhi watu

Akizungumza leo mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Frida Mokiti, amesema hali za watu hao zinaendelea vizuri isipokuwa mgonjwa mmoja hali yake siyo nzuri kutokana na kusagika mfupa wa mguuni na hivyo wanawasiliana na Wizara ya Afya ili kupata maelekezo ya kufanya.

Hata hivyo amesema kati ya wagonjwa hao watano walitibiwa na kuruhiswa wengi wao wakiwa wamechubuka kidogo na wengine kupata mshituko, na 11 waliobaki wapo wodini Mount Meru ambapo wanaume wapo nane na wanawake watatu.

Katika hatua nyingine kikosi cha wakaguzi wa mabomu kilifika eneo la tukio asubuhi ya leo na kufanya kazi yao ya ukaguzi wakiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.