Jumatano , 21st Jan , 2015

eshi la polisi mkoa wa Morogoro limewafikisha mahakamani madereva wa bodaboda 11 waliobainika kuhusika na matukio ya kuvamia wafugaji.

Hofu imeendelea kutanda kwa wafungaji mkoani Morogoro kufuatia bodaboda kuendelea kuwavamia na kuwapora wafugaji kila wanapoonekana katika mji wa Morogoro kwa madai ya kulipiza kisasi baada ya mkulima mmoja kuuwawa katika bonde la Mgongola ambapo wafanyabiashara, wafugaji na wanaofanya shughuli za ulinzi wamelazimika kuukimbia mji wa Morogoro na baadhi ya wanafunzi wa vyuo kurudi majumbani.

Wakizungumza wakiwa porini kujadili hatma ya usalama wa wafugaji  hao wakiwemo wanaume kwa wanawake kutoka wilaya za Kilosa na Mvomero wamesema hawakuusika na mgogoro uliosababisha mauaji ya mkulima katika bonde la Mgongola na hivyo kuomba serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama wawasaidie  kwani hivi sasa wagonjwa wanalazimika kutibiwa majumbani wanafunzi hawaendi shule kwa kuhofia madereva wa bodaboda.
 
Nao baadhi ya wafugaji waliojeruhiwa na kuporwa fedha wameeleza jinsi walivyovamiwa na kupigwa kisha kunyanganywa simu na fedha na hivi sasa wanaugulia majumbani na wanashindwa kwenda hospitali kupata matibabu kwa hofu ya kuvamiwa na madereva wa bodaboda huku baadhi ya wanafunzi wafugaji wanaosoma chuo cha St Josefu Morogoro nao wameelezwa kurudi majumbani.
 
Wakati haya yakitokea jeshi la polisi mkoa wa Morogoro limewafikisha mahakamani madereva wa bodaboda 11 waliobainika kuhusika na matukio ya kuvamia wafugaji ambapo wamesomewa mashitaka mawili ya kuvamia wafugaji kwa nyakati tofauti mbele ya hakimu mkazi Maua Hamduni ambapo washtakiwa wamenyimwa dhamana kwa hofu ya usalama wao na kurudishwa rumande .