
Katika vitongoji vya makazi, waandamanaji waliwarushia mawe polisi, walifunga barabara na kuchoma matairi. Jeshi lilishika doria mitaani huku polisi wakiwarushia mabomu ya machozi waandamanaji hao, kuwakagua na kuwaweka kizuizini watu wanaodaiwa kusababisha fujo.
Umoja wa Afrika (AU) na jumuiya ya uchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi (Ecowas) zimeshutumu vikali ghasia zilizozuka Ijumaa nchini Senegal baada ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko kupewa kifungo cha miaka miwili kwa kosa la ‘kupotosha vijana’.
Katika taarifa yake mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika Moussa Faki , amesema matendo ya Senegal yanachafua taswira ya demokrasia ya nchi ambayo kwa miaka mingi Afrika imekuwa ikijivunia na amewahimiza viongozi wote wa kisiasa kutumia hekima na mashauriano kutatua zogo hili.
Mapigano hayo yalizuka kwa mara ya kwanza Alhamisi, baada ya Sonko kukutwa na hatia ya kupotosha vijana lakini akaachiliwa kwa tuhuma za kumbaka mwanamke aliyekuwa akifanya kazi katika chumba cha masaji na kutoa vitisho vya kifo dhidi yake. Sonko hakuwepo mahakamani wakati wa kutolewa kifungo hicho na hakimu ameagiza kuwa akamatwe punde akionekana hata hivyo Wakili wake amesema kibali bado hakijatolewa cha kukamatwa kwake.
Wafuasi wake wanahofia kuwa kifungo hicho ni njama ya kumzuia kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.Chini ya sheria za Senegal, hukumu ya Sonko itamzuia kugombea katika uchaguzi wa mwaka ujao, alisema Bamba Cisse, wakili wa utetezi. Hata hivyo, serikali ilisema kuwa Sonko anaweza kuomba kesi isikilizwe upya mara tu atakapofungwa. Haikufahamika ni lini atawekwa kizuizini.
Sonko aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa urais wa Senegal 2019 anachukuliwa kuwa mshindani mkuu wa Rais Macky Sall katika uchaguzi wa urais wa 2024, ingawa Sall hajathibitisha au kukana kutaka kuchaguliwa tena.