Alhamisi , 30th Jun , 2016

Mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Kanali Chiku Galawa amesema mkoa huo umeweka mpango mkakati maalumu wakuwashirikisha wadau mbalimbali nchini ili kuhakikisha wanasimamia sekta ya elimu katika mkoa huo ili kuwezesha sekta hiyo ikuwe kwa kiwango kikubwa.

Luteni Galawa ameyasema hayo wakati akizungumza na East Africa Radio kuhusu mipango ya kuinua elimu katika mkoa huo ambao ni mpya sambamba nakuboresha mazingira ya elimu kwakuhakikisha miundombinu ya kufundishia inaboreshwa kwa ushirikiano baina ya serikali na wananchi.

Amesema mipango hiyo inaanzia kwa shule za msingi hadi sekondari na ameitaka jamii kuendelea kuboresha mazingira ya shule kwakukubaliana wenyewe kwa kutoa huduma mbalimbali kama chakula na vifaa mbalimbali vya shule ili kuhakikisha wanafikia malengo ya kitaifa na yale ya mkoa wa Songwe waliyojiwekea.

Amesema ni wajibu kwa wazazi, walezi na wanafunzi wote kuitumia fursa ya elimu bure ambayo inatolewa na serikali kwakuwa matatizo ya msingi yaliyokuwa yakikwamisha upatikanaji wa elimu bora yanaendelea kutatuliwa kila wakati.

Ameongeza Sera ya Elimu bure ni ukombozi kwa watanzania wote na maendeleo ya sekta ya elimu kwa ujumla nchini, kwamantiki hiyo kila mdau wa elimu anapaswa kuielewa dhana hiyo nakusaidia utekelezaji wake ili kila mwanafunzi nchini apate kuitumia fursa ya elimu bure kwa maendeleo yake na maendeleo ya taifa zima.