Alhamisi , 14th Jan , 2016

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imetahadharisha watu wanaouza mafuta ya Petroli kiholela majumbani kwani kunaweza kusababisha hatari ikiwemo milipuko ambayo inaweza kusababisha madhara.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo.

Hayo yameelezwa na Afisa Habari na Mawasiliano EWURA, Titus Kaguo katika mkutano na Wadau wa Nishati na Maji nchini, na kuwataka wauzaji kuzingatia kanuni za usalama ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.

Titus amesema kuwa kutokana na kuongezeka kwa usafiri wa pikipiki maarufu kama boda boda kumepelekea kuanzishwa kwa vituo vingi ambavyo si rasmi hasa majumbani jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama.

Mkurugenzi wa wa Idara ya Petroli EWURA, Godwin Samwel amesema kuwa serikali ina mpango wa kuhakikisha watanzania wengi wanatumia nishati ya gesi ili kunusuru mazingira kwa kuepuka matumizi ya mkaa na kuni ambayo huaribu mazingira.

Kwa upande wao wadau wa biashara ya mafuta Christopher Kamwana na Abulaziz Hussein wameeleza changamoto inayowakabili ni pamoja na sera ambazo huchangia kuzorotesha biashara ya mafuta ikiwemo ukaguzi wa NEMC unaofanyika kabla ya kuanzisha kituo.

Suala la uchakachuaji wa mafuta ni changamoto ambayo imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi zinazofanywa na EWURA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.