
Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania, Filberto Cerian Sebregondi.
Balozi Sebregondi amesema hayo leo katika mahojiano na East Africa Televisheni na Radio, wakati akizungumzia masuala mbali mbali yanayohusu maadhimisho ya wiki ya Umoja wa Ulaya, yatakayoanza Mei nane mwaka huu.
Katika mahojiano hayo, balozi Sebregondi amesema ni kawaida kwa michakato ya katiba kupitia vipindi vigumu vya tofauti kama zilivyoonekana kwenye bunge maalumu la katiba na kwamba hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kunapatikana katiba nzuri inayotarajiwa na wananchi.
Aidha balozi Sebregondi amezungumzia masuala mbali mbali yanayohusu jumuiya ya Afrika Mashariki na kuonyesha imani yake kuwa jumuiya hiyo inaweza kuwa imara na kufikia shirikisho la kisiasa iwapo nchi wanachama zitafuata na kutekeleza misingi ya kuanzishwa kwake.
Amefafanua kuwa jumuiya ya Ulaya imekuwa ikifadhili jumuiya hiyo hasa katika ujenzi wa miundombinu imara ya usafirishaji wa mizigo na bidhaa pamoja na uonishaji wa sera na sheria baina ya nchi wanachama, na kwamba mafanikio zaidi ya kiuchumi yanaweza kupatikana iwapo jumuiya ya Ulaya itafikia muafaka wa makubaliano ya kiuchumi yajulikanayo kama Economic Partnership Agreement (EPA) ambayo majadiliano yake kwa sasa yapo katika ngazi ya mawaziri.