Alhamisi , 14th Mei , 2015

Sakata la kusafishwa kwa waliohusika na ubadhirifu wa mamilion katika Tegeta Escrow na ukiukaji wa haki za Binadamu katika operesheni tokomeza limeibuka bungeni.

Mbunge wa Kigoma Mjini Peter Serukamba.

Mbunge wa Kigoma Mjini Peter Serukamba ametaka kujua ni vigezo gani vilivyotumia kuwasafisha baadhi na kuwaacha wengine.

Akichangia hotuba ya mwelekeo wa kazi za serikali makadiro ya matumizi ya fedha ya ofisi ya waziri mkuu na bunge kwa mwaka 2015/2016 Serukamba amesema inashangaza kamati iliyochunguza tuhuma kukuta wahusika ni wasafi.

Mh. Serukamba amesema hakubaliani na jinsi suala hilo lilivyoshughulikiwa na na kuhoji kwanini watu wengine wafikishwe mahakamani waondolewe nyadhifa na wengine wakiwa bado wapo maofisini.

Aidha Mh. Serukamba alimtaka Katibu Mkuu, Balozi Ombeni Sefue kutangaza kuwa wengine waliotuhumiwa kuwa ni wachafu kama Prof. Anna Tibaijuka, Andrew Chenge, na Jaji Fredrick Werema nao wasafishwe.

Pia Serukamba amesema iwapo waliosafishwa ni wasafi na muamala uliofanyika ulikuwa ni safi basi waliojiuzulu warejeshwe kwenye nafasi zao huku akitaka iundwe tume ya kuwasafisha viongozi waliojiuzulu kwa kashfa za nyuma ikiwemo waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa ili nao wasafishwe na warejee katika nafasi zao.