
Rais wa Nigeria Bola Tinubu amependekeza kipindi cha mpito cha miezi tisa kwa serikali ya Niger kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kiraia.
Bw Tinubu alisema Niger inaweza kuiga mfano wa mtawala wa zamani wa kijeshi wa Nigeria Jenerali Abdulsalami Abubakar, ambaye alirejesha nchi hiyo katika utawala wa kidemokrasia mwaka 1999 baada ya miezi tisa kama kiongozi wa junta.
Bw Tinubu, ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Magharibi ya Ecowas, alisema mfano wa Nigeria umethibitisha mafanikio makubwa, na kuiongoza nchi hiyo katika zama mpya za utawala wa kidemokrasia.
Serikali ya Niger imetangaza kipindi cha mpito cha miaka mitatu ambacho kimekataliwa na Ecowas.
Bwana Tinubu alizungumza wakati akiwakaribisha viongozi wa Kiislamu ambao wamekuwa katika ziara mbili nchini Niger kwa mazungumzo na junta.
Alisema Ecowas haitaondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Niger hadi pale serikali ya nchi hiyo itakapofanya mageuzi chanya.