Alhamisi , 12th Mar , 2020

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga, amezijibu tuhuma alizozitoa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, kuhusu madai ya vifo vya watu 13 mkoani Singida kwamba walichinjwa na mmoja kuchomwa moto na Serikali haikuchukua hatua zozote.

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga

Akizungumza leo Machi 12, 2020, DPP Mganga amesema kuwa taarifa alizozitoa Lema zimeleta taharuki kwa Watanzania na kuwafanya wasiishi kwa amani na kwa jambo hilo lazima atalichukulia hatua na kwamba alichokisema Mbunge Lema ni kauli za kisiasa, kwani matukio hayo yote yalikwishachukuliwa hatua stahiki.

"Na kama yeye aliona hawa wamechinjwa na anawajua waliowachinja kwa mujibu wa sheria yeye anawajibika kutoa taarifa Polisi, Lema naomba ajitokeze aje kuniambia ni lini alienda kutoa taarifa kwamba kuna watu wanachinjwa na hatua hazikuchukuliwa" amesema DPP Biswalo Mganga.

Aidha DPP Mganga ameongeza kuwa "Tunapochukua hatua mnielewe, hatuwezi kuendelea kuwa Taifa la watu wenye uzushi, kwa hili nitachukua hatua, hatuwezi kuendelea kuwa na upotoshaji wa namna hii, halafu watu wanasema wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaonewa wakati wanafanya upuuzi".