Jumatatu , 29th Mei , 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia mipaka na majukumu yao katika utendaji wa kazi ili kuepusha migogoro na miingiliano katika kuwahudumia wananchi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Aidha Makamu wa Rais amewasihi viongozi hao kutambua lengo kuu katika nyadhifa zao ni kuwaletea wananchi maendeleo na siyo migogoro baina yao hivyo ni muhimu kuheshimiana, kuwajibika, kushirikiana kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuondoa vikwazo vyovyote vinavyoweza kukwamisha miradi hiyo.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa Mapato na kudhibiti uvujaji wa mapato katika maeneo yao, ambapo ametaja tathmini ya taarifa za mapato kutoka katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na vyanzo vingine vilivyokusanywa kupitia mashine za POS imebaini katika baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa fedha hazipelekwi katika akaunti husika za benki hivyo amewasihi kuzingatia taratibu za fedha na kudhibiti matumizi yasiyo na tija.