Ijumaa , 23rd Feb , 2024

Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango ameagiza kuanzishwa kwa mafunzo ya ufugaji wa samaki maramoja katika chuo cha ufundi stadi VETA katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga ili kuendana na shughuli za kiuchumi za wananchi wa eneo hilo ambapo amemuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi kusimamia pia.

Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango

Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango ametoa maagizo hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika chuo cha ufundi Standi (VETA) Wilayani Mkinga mkoani Tanga na kusisitiza chuo hicho kuongeza mafunzo ya ufugaji wa samaki ili kuendana na shughuli ya uvuvi inafonywa na wakazi wa eneo hilo. 

"Haya mafunzo yanayotolewa katika chuo hiki ni muhimu sana yaendane na shughuli za kiuchumi za wananchi wa eneo hili katika hili ninamtaka Waziri wa mifugo na uvuvi alisimamie kuhakikisha kwamba chuo hiki cha Veta kinawezeshwa kuanzishwa kozi ya ufugaji wa samaki mara moja, "alisisitiza Dkt Mpango. 

Aidha Dkt Mpango akatoa ombi kwa Sekta zote binafsi nchini kuwapatia nafasi wanafunzi wa VETA ili waweze kufanya mazoezi kwa vitendo na hatimaye waweze kukuza ujuzi wao.

Mwakilishi wa jimbo la Mkinga na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula ametoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita kwa kuleta maendeleo yanayoonekana katika Wilaya hiyo.

Prosper Mgaya ni Mkurugenzi Mkuu wa Veta Tanzania amesema chuo hicho kwa sasa kimeanza na fani tatu na kina idadi ya wafunzi 78 ambapo wanafunzi 48 ni wa mafunzo ya muda mrefu na wanafunzi 34 wa mafunzo ya muda mfupi. 

Chuo hicho kimegharimu shilingi Billioni 2.6 na kina jumla ya majengo 17 yenye uwezo wakubeba wanafunzi 240.