Jumanne , 27th Sep , 2016

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amemwagiza meneja wa Tanesco, mkoa wa Manyara Gerson Manase, kupeleka huduma za shirika hilo kwa wananchi vijijini, badala ya kukaa ofisini kuwasubiri wateja wawafuate.

Dkt. Merdard Kalemani

Akitoa agizo hilo jana katika kijiji cha Losinyai na Kilombero wilayani Simanjiro, ambako ametembelea kukagua miradi ya wakala wa umeme vijijini (REA), aliagiza pia ifikapo jana saa 8:00 mchana umeme umewashwa na endapo hautawashwa apigiwe simu ili amwajibishe meneja na mkandarasi wa kazi hiyo.

Dkt. Kalemani amesema inasikitisha kuona wananchi wanatumia gharama kubwa kufuata huduma kwenye ofisi za Tanesco za ulipaji wa malipo ya masuala ya umeme, wakati wao ni wateja wanapaswa kupelekewa huduma hiyo mahali walipo, kwani wao ni wafalme.

Aidha aliagiza wakala wa usambazaji umeme vijijini wilayani Simanjiro, Yared Zhang wa kampuni ya CCC Nigeria, kuwalipa wafanyakazi waliomsaidia kusambaza vifaa vya umeme vijijini fedha zao ambazo sasa wanadai zaidi ya shilingi milioni 13, kabla ya Septemba 30 mwaka huu.

Pia ametumia fursa hiyo kuwazawadia wazee wawili ambao ni Elias Lukumay wa kijiji cha Kilombero na Looki Kimbele wa kijiji cha Losinyai, kifaa maalum kiitwacho umeta ambacho hakihitaji kufunga nyaza za umeme ndani ya nyumba ukifunga hicho tu yatosha kuwashiwa umeme.

Naye mkuu wa wilaya ya Simanjiro,Mhandisi Zephania Chaula, amesema wananchi wasiopata umeme awamu ya pili REA wasilalamike watapata awamu ya tatu na waliopata umeme huo watumie kwa kubuni ufunguaji viwanda vya nyama na maziwa, sababu maeneo hayo yana mifugo mingi.

Kwa upande wa wananchi kupitia risala yao iliyosomwa na Grace Mboya ambaye mwalimu mkuu wa shule ya msingi Losinyai, amesema changamoto kubwa katika mradi huo ni wafanyakazi wa REA kutolipwa stahiki zao pamoja na baadhi ya vijiji kutofikiwa na mradi.