Alhamisi , 1st Jun , 2023

Mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah amekiomba Chama cha Mapinduzi mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Wizara husika, kuwahamisha watumishi waliokaa muda mrefu katika wilaya hiyo ambao baadhi yao hawatekelezi majukumu yao na badala yake wamekuwa wakifanya kazi zao binafsi.

Mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa sokoni ambao mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abrahamani  Abdalah (MNEC), mkuu huyo wilaya amesema kukaa kwao muda mrefu kumewafanya kutotimiza majukumu yao ipasavyo jambo linalokwamisha maendeleo wilayani humo. 

DC Zainabu amesema pamoja na jitihada nzuri za Rais, alikiri akiwa msimamizi wa shughuli za serikali Pangani kuna changamoto za baadhi ya watumishi hawatekelezi majukumu yao na badala yake wamekuwa wakifanya kazi zao binafsi ikiwemo kusimamia bodaboda na kusimamia masuala yao ya kifedha

"Mheshimiwa Mwenyekiti changamoto ya pili ni serikali kuwaleta watumishi walioharibu sehemu nyingine wanaletwa hapa Pangani siyo sehemu ya majaribio, tunataka watumishi wenye utayari wa kuwahudumia wananchi na kusikiliza kero zao, lakini siyo kuwa na watumishi wasiotekeleza wajibu wao," amesema DC Zainabu

Hata hivyo, alisema ,akiwa msimamizi mkuu wa shughuli za serikali hatafanya mzaha na mtumishi yeyote ambaye atakayerudisha nyuma maendeleo ya wananchi na alisema atampatia majina ya watumishi hao wanaoshindwa kwenda na kasi ya maendeleo ya wilaya hiyo kwa sasa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa, alisema kuwa Pangani ile ya zamani siyo ya sasa, Pangani ya sasa inapiga hatua za maendeleo tangu mbunge Jumaa Aweso awe mbunge ambapo serikali imekuwa ikileta fedha nyingi za maendeleo.