Ijumaa , 11th Oct , 2019

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Gabriel Daqaro, amemtaka Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, kuacha kutafuta huruma kwa watu ambao hawajahusika katika sakata lake la kuzuiwa kufanya mikutano jimboni mwake.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Gabriel Daqaro na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.

Hayo ameyabainisha leo Oktoba 11, 2019, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, ambapo amesema kuwa kitendo cha Mbunge huyo kuhusisha masuala yake ya kisiasa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya si jambo sahihi hata kidogo kwakuwa yeye hahusiki na kutoa vibali vya mikutano ya wabunge, kwani jukumu lake kubwa ni kuhakikisha usalama wa wananchi wake.

''Aende polisi akafafanuliwe, aache kulalamika na kusingizia watu, mimi Mkuu wa Wilaya napata wapi muda wa kukutana na mbunge, nafanya shughuli zangu wilaya iwe salama, na je anao ushahidi kama mimi nilihusika hadi yeye aandikiwe barua ya kusimamishwa mikutano yake, aende kwenye mamlaka kuliko kuanza kutafuta huruma zisizo na misingi'' amesema DC Daqaro.

Kwa upande wake Mbunge Lema, amesema kuwa yeye anao ushahidi kama Mkuu huyo wa Wilaya alihusika ili kupewa barua ya kusimamishwa kufanya mikutano ya kuongea na wananchi wake, lakini leo ameongea na Kamanda wa Polisi Mkoa na amemruhusu kuendelea na mikutano yake kama kawaida.

''Barua ya kuzuia mikutano iliyokuwa imeandikwa ni barua iliyokuwa imejaa utoto na mimi nimekutana na OCD anatoka ofisini kwa DC baada ya kuleta hiyo barua na nikata kuongea naye akashuka kwenye ngazi kama anadondoka, sasa nimefuatilia kwa wakubwa wao na nimetoka kwenye ofisi ya Mkuu wa Polisi Arusha na mikutano yetu itaendelea kama kawaida'' amesema Lema.

Hatua hii imekuja baada ya hapo jana Oktoba 10, 2019, Mbunge Lema kutoa kauli inayomzungumzia Mkuu wa Wilaya ya Arusha, kwamba anahusika katika masuala ya yeye kuzuiwa kufanya mikutano yake, baada ya kupokea barua ya katazo la kufanya mikutano, kutoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha.