Alhamisi , 31st Jul , 2014

Matangazo ya waganga wa kienyeji na wapiga ramli yameendelea kuonekana katika maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam, licha ya serikali kupitia kwa waziri wa afya na ustawi wa jamii Dkt Seif Rashid kuagiza kuondolewa kwa matangazo hayo.

Moja ya matangazo ya waganga wa kienyeji yaliyosambaa katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam.

Matangazo ya waganga wa kienyeji na wapiga ramli yameendelea kuonekana katika maeneo kadhaa katika manispaa za jiji la Dar es Salaam, licha ya serikali kupitia kwa waziri wa afya na ustawi wa jamii Dkt Seif Rashid kuagiza kuondolewa kwa matangazo hayo haraka iwezekanavyo.

Uchunguzi wa East Africa Radio umebaini kuwepo kwa matangazo hayo ambayo kwa mujibu wa baraza la taifa la tiba asili na tiba mbadala, uwepo wake ni ukiukwaji mkubwa sheria kama anavyoeleza Mratibu wa Shirikisho la Tiba Asili nchini Tanzania Bw. Boniventura Mwalongo.

Mwalongo amesema kuna haja ya mamlaka hizo kusimamia uondoaji wa matangazo hayo haraka ili kuepusha ukiukwaji mkubwa wa sheria kupitia utapeli na uhalifu unaofanywa na wapiga ramli na waganga wa kienyeji nchini.

Wakati huo huo, Askofu mkuu kanisa la Pentekoste PAGT, Mhashamu Daniel Alley amemshauri Rais Jakaya Kikwete kusitisha kwa muda mchakato wa katiba mpya kutokana na kutokuwepo kwa uwezekano wa kukamilika kwa zoezi hilo kabla ya uchaguzi mkuu mwakani.

Askofu Alley amesema hayo jana mjini Kigoma na kuongeza kuwa mchakato wa bunge la katiba umegubikwa na malumbano ya vyama mabayo hayatoi fursa kwa kukamilika kwa katiba mpya na badala yake ni fedha za watanzania zimekuwa zikiteketea kinyume na matarajio.

Aidha Askofu Alley amevitaka vyama vya siasa kutoingilia mchakato na kupeleka mawazo ya vyama vyao kwa kuwa katiba inayotungwa ni ya wananchi na si ya vyama vyao.