Jumatatu , 11th Jan , 2016

Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambaye pia ni katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar ni batili na ni agenda ya chama kilichoshindwa na haina uhalali wowote kisheria.

Seif ameyasema hayo hii leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu hatma ya kisiasa ya Zanzibar baaada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar ZEC kupitia kwa mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar na kubainisha kuwa ungetangazwa tena ndani ya siku 90.

''Mimi nasema hakuna uhalali wa kisheria wa kurudia uchaguzi huu kwani katiba ya Zanzibar ibara ya 28(2) inabainisha wazi kuwa muda wa urais ni miaka 5 tuu''

''Pili uchaguzi ukirudiwa tutakuwa hatuwajengi wananchi vizuri katika kuwa na imani kwa mamlaka zilizowekwa, tatu uchaguzi hauwezekeni kwa sababu tume ya uchaguzi kupitia mwenyekiti wake imeonesha dhahiri kushindwa kazi na haiwezi kuaminika kwa wananchi''Amesisitiza Malim Seif.

Pia Maalim Seif ameeleza kuwa kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kumeleta athari kubwa sana kama vile mgogoro wa kikatiba, serikali kuendelea kufanya kazi mbalimbali tena nyingine za uteuzi vilevile kumewaweka wananchi katika sintofahamu juu ya mustakakabali wa maisha.

Aidha Maalim Seif amependekeza kwamba ili kuleta muafaka wa kisiasa Zanzibar na wananchi wawe huru na kazi zao ni bora matokeo halali ambayo yalionyesha Maalim Seif kupata 52% na Dr. Shein kupata 46% yatangazwe ili serikali ya umoja wa kitaifa iundwe kwa kuzingatia misingi ya kisheria.