
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe akiwa na viongozi mbalimbali wa Chama hicho.
Hii inakuwa ni mara ya 6 sasa kuahirishwa kwa kesi hiyo. Hakimu Mkuu Mkazi, Wilbard Mashauri ametoa amri ya kuahirishwa kwa keshi hiyo baada ya mshtakiwa namba 2 katika kesi hiyo, Peter Msigwa kutokuwa na uwakilishi wa kisheria huku mshtakiwa namba 5 Esther Matiko akishindwa kuhudhuria mahakamani kwa sababu ya matatizo ya kiafya.
Wakili wa utetezi Peter Kibatala ameiambia mahakama kuwa yeye anawakilisha washtakiwa nane kati ya tisa katika kesi hiyo, isipokuwa mshtakiwa namba 2 ambaye ni Mchungaji Peter Msigwa. Alipopewa nafasi ya kujieleza, mshtakiwa huyo aliiomba mahakama hiyo impatie muda wa wiki tatu kutafuta wakili wa kumtetea baada ya wakili wake Jeremiah Mtobesya kuondoa uwakilishi wake katika shauri hilo.
Itakumbukwa kuwa Agosti 23, mwaka huu wakili wa upande wa utetezi, Mtobesya alijitoa katika kesi hiyo ambapo alidai mbele ya mahakama kuwa haoni haki ikitendeka katika shauri hilo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe(Mb), Katibu Mkuu wa Chama, Dkt. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Bara, John Mnyika (Mb) na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Zanzibar Salum Mwalim.
Wengine ni Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa, Halima Mdee (Mb), Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama John Heche(Mb), Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Peter Msigwa(Mb), Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Esther Bulaya (Mb) na Mweka Hazina wa BAWACHA Taifa, Esther Matiko (Mb).