Ijumaa , 9th Jun , 2023

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Cheng Mingjian na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu kuimarisha na kudumisha urafiki na udugu, kati ya CCM, serikali ya Tanzania na China.

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo akiwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Cheng Mingjian

Katibu Mkuu Ndugu Chongolo na Balozi Mingjian, wamezungumzia umuhimu wa pande hizo mbili kuendelea kutengeneza fursa za kubadilishana uzoefu katika masuala ya elimu, mafunzo, biashara, uwekezaji, uongozi, utawala, mapambano dhidi ya rushwa na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

"Nchi za Tanzania, kama ilivyo vyama vinavyoongoza katika nchi hizi, kwa maana ya CCM na Chama cha Kikomunisti cha Watu wa China (CPC), vivyo hivyo kwa serikali zinazoundwa na vyama hivi, serikali ya China na CCM, ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni pande mbili ambazo zimekuwa na urafiki ambao sasa ni udugu wa muda mrefu, katika shida na raha," amesema Chongolo

Aidha Chongolo ameongeza kuwa "Na kwa namna hadhi ya ushirikiano wa pande hizi ilivyoongezeka na kupanda, hasa kufuatia ziara ya kihistoria ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya mwaliko wa Mhe. Xi Jinping, Rais wa China, ni muhimu kuendelea kukutana na kuzungumza ili kuboresha, kuimarisha na kudumisha ushirikiano wetu katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kupeana fursa za mafunzo ya uongozi kwenye mambo mbalimbali,".

Kwa upande wake, Balozi wa China, Mhe. Mingjian amemhakikishia Chongolo kuwa nchi na serikali ya China anayoiwakilisha hapa nchini, inauchukulia urafiki na udugu wa pande hizo mbili kuwa wa kipekee na iko tayari kuendelea kuuenzi na kuudumisha kwa ajili ya manufaa ya watu wa Tanzania na China.