Jumatatu , 6th Mei , 2024

Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga kimevitaka vyama vya siasa nchini kuacha kukosa na kunyoshea Serikali kidole kana kwamba haijafanya kitu huku wakisema wanapaswa kuunga mkono jitihada zinazofanywa katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya,  elimu na sekta ya maji.

Rajab Abrahaman Abdalah, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga Rajab Abrahaman Abdalah wakati akizungumza na wakazi wa jiji la Tanga kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Makorora ikiwa zimepita siku chache tu tangu kufanyike maandamano ya CHADEMA jijini humo yakifuatiwa na mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mwenyekiti wake wa Taifa Freeman Aikael Mbowe.

Kwa mujibu wa Abrahman amesema Serikali ya CCM ni sikivu na imekuwa ikifanya mambo makubwa ambayo yamechangia kuharakisha maendeleo ya wananchi huku akiwasihi wananchi kuendelea kukiunga mkono chama tawala na kuepuka propaganda za Chadema na vyama vingine vya upinzani. 

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Tanga alisema, Mbowe alipaswa kuwashauri na kuwaongoza wananchi katika kuunga mkono juhudi za serikali badala ya kuwashawishi katika kudharau mazuri yanayofanyika.

Alimshangaa Kiongozi huyo Chadema Taifa kwa hatua yake ya kusema anakusudia kuweka mizizi Tanga kwa lengo la kuwashawishi wananchi kuwaunga mkono badala ya kuonesha utayari wa kuungana na Serikali ili kuharakisha maendeleo ya wananchi walio wengi.

Aidha, Mwenyekiti Rajab alisema kuwa viongozi wa vyama hivyo vya upinzani badala ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayoendelea kuzifanya  katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo,  wao wamekuwa wakipita kuwadanganya na kuwarubuni wananchi juu maendeleo  jambo ambalo sio sawa.   

"Mimi niwaambie kuwa wanawadanganya kweli kwa kuwa hata wao pia ni wana ccm wenzetu na hata Mbowe ni mwanachama mwenzetu wa chama cha mapinduzi tunakaa naye mpaka kwenye vikao vyetu vya ndani vya siri wakija huku kwenu wananchi wanawadanganya niwaombe msidanganyike wasiwarubuni si wao tu viongozi wote wa vyama vya upinzani ni wanachama wa chama cha mapinduzi, "alisisitiza Mwenyekiti Rajab. 

"Wapo vijana wenzetu kuanzia asubuhi mpaka jioni wao wapo maskani ni kudanganyana kuelezana habari za uongo kutaka serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania imletee fedha mfukoni ndugu zangu hakuna serikali hiyo dunia nzima inayowapa watu fedha mfukoni kazi ya serikali ni kuweka miundombinu mizuri ili kuweza kuajiri watu na kuwawezesha watu kujiajiri wenyewe ili wajiingizie kipato, "alisema Mwenyekiti Rajab.