Ijumaa , 19th Dec , 2014

Chama  cha Mapinduzi  wilaya  za Rorya na Musoma mkoani Mara  wamemtaka  waziri  mwenye dhamana na serikali za mtaa kuchukua hatua za haraka kwa wakurugenzi  wa halmashauri hizo  kabla ya kuitisha maandamano.

Chama  cha Mapinduzi  wilaya  za Rorya na Musoma mkoani Mara  wamemtaka  waziri  mwenye dhamana na serikali za mtaa kuchukua hatua za haraka kwa wakurugenzi  wa halmashauri hizo  kabla ya kuitisha maandamano ya kuwatoa katika ofisi zao  kwa madai ya  kuvuruga  zoezi  zima  la  uchaguzi  wa serikali za mitaa.
 
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Rorya Samwel Kiboye, amesema pamoja na kulalamika kuhusu kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi huo ambao umefanyika Jumapili iliyopita lakini ofisi ya mkurugenzi ilishindwa kurekebisha kasoro hizo hatua ambayo amesema imesababisha uchaguzi huo kuvurugika.
 
Hata hivyo mwenyekiti  huyo  ameshauri  tume ya taifa ya uchaguzi  kufikiria kutumia  askari ambao  wamepata mafunzo  ya jeshi la kujenga  taifa kusimamia uchaguzi  huo badala ya watendaji  wa serikali  ambao  amedai  wengi  wao  wamekuwa wakitumiwa na vyama vya siasa.

Naye Katibu  wa  CCM wilaya ya Musoma Jacob Nkomoro, akitoa tathimini ya uchaguzi huo, ameitaka serikali kupitia waziri mwenye dhamana  ya serikali za mitaa kuchukua hatua  za haraka  kumuwajibisha  mkurugenzi   mtendaji  wa manispaa hiyo  kwa  madai  ya kushindwa  kusimamia  vema uendeshaji  wa uchaguzi huo hatua ambayo imefanya taratibu nyingi kukiukwa.