Alhamisi , 11th Jul , 2024

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea kusimamia mkakati wake maalum wa kuzuia vitendo vyote vya kihalifu katika jiji la Dar es Salaam. Tarehe 28 Juni 2024 lilimkamata na kumuhoji kwa kina Mussa Khamis Bakari @buda (30) wakala wa Forodha,

Mkazi wa Temeke kwa tuhuma za mauaji ya Abdallah Twahir Selemani ambaye alikuwa rafiki yake na baada ya kumuua alifanikiwa kuiiba pesa za marehemu Tsh Milioni 61 kutoka kwenye akaunti ya huyo rafiki yake.

Taarifa fupi za tukio ni kuwa  tarehe 1 Mei, 2024 majira ya saa 10:20 asubuhi huko maeneo Mbutu Kichangani, Kigamboni pembezoni mwa barabara itokayo Cheka kuelekea beach ya Kichangani uliokotwa mwili wa mtu mmoja mwanaume akiwa ameshafariki na baadae mwili huo ulitambuliwa kuwa ni Abdallah Twahir Selemani mkazi wa Chanika.

Awali tarehe 4 Mei 2024 Jeshi la Polisi lilipokea taarifa ya kupotea kwa Abulllah Twahir Selemani kutoka kwa mama yake kuwa alipotea katika mazingira ya kutatanisha. Uchunguzi wa Jeshi la Polisi baadae uligundua kuwa tarehe 30 Aprili 2024 mtuhumiwa Mussa Khamis Bakari @buda alikuwa na marehemu wakitumia gari namba T.928 DFY Suzuki Kei wakitokea Magomeni kuelekea Temeke, Kijichi mpaka eneo ulipokutwa mwili wa marehemu. Uchunguzi wa vitu mbalimbali umebainisha mtuhumiwa alimuua  na baadae kwenda kutupa mwili huo pembezoni mwa barabara ulipookotwa .

Baada ya kumuua, mtuhumiwa alichukua kadi ya benki ya marehemu na kwa nyakati tofauti tofauti alianza kutoa  pesa kiasi cha shilingi Milioni 61 kutoka kwenye akaunti ya marehemu. Chanzo cha mauaji ni tamaa ya kutaka kuiba pesa kutoka kwa rafiki yake ambaye sasa ni marehemu. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

Katika tukio lingine Jeshi la Polisi limefuatilia  matukio ya unyan’ganyi na wizi wa pikipiki katika Jiji la Dar es Salaam na kufanikiwa  kuwakamata watuhumiwa 23 na  pikipiki 39 zilizoibwa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia mbinu ya kujifanya abiria  na wakifika  njiani hujitokeza watu wengine ambao humtishia dereva kwa mapanga kumjeruhi na kumuibia pikipiki hiyo, wakatii mwingine  pikipiki zinazokuwa zimeegeshwa nje hutumia mbinu ya kuunganisha waya, kuwasha na kuiba pikipiki hizo.

Ufuatiliaji wa Jeshil la Polisi umebaini watuhumiwa hao baada ya kuziiba pikipiki wamekuwa wakiziuza kwa gharama nafuu mikoa mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Dodoma na Singida.

Ufutiliaji huo umefakiwa kukamata risiti za kugushi 18 za kusafirishia pikipiki za wizi, kadi 11 za usajili wa pikipiki za kugushi, kadi (03) za usajili wa magari za kugushi, vyeti mbalimbali vya kuzaliwa na kimoja cha ndoa vya kugushi, plate number (03)  za pikipiki, kitabu kimoja cha bima ya magari, nyaraka mbalimbali za TRA, barua mbalimbali  zenye nembo za jeshi la Polisi Tanzania, mihuri mbalimbali ya manispaa ya Kinondoni,Temeke, IIala, Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, RITA, Mamlaka ya Bandari na mhuri mmoja wa moto ulioandikwa "United Republic of Tanzania" wenye nembo ya bibi na bwana, leaf 56 za kutengenezea kadi za vyombo vya moto, leaf 86 za kutengenezea vyeti vya vizazi na vifo vyenye nembo ya msajili wa vizazi na vifo.

Wakati huo huo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linakanusha taarifa ya sauti inayosambaaa kwenye mitandao ya kijamii ikielezea kuwepo kwa tukio la mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kutekwa nyara maeneo ya kituo cha kontena kilichopo ndani ya chuo hicho na watu wasiojulikana wakitumia usafiri wa bajaji kisha kupelekwa Kimara na baadae kutelekezwa eneo la Masaki.
Jeshi la Polisi limefanya ufuatiliaji wa taarifa hiyo  na kubaini kuwa ujumbe huo wa sauti ni wa muda mrefu  zaidi ya miaka mitano nyuma na uliwahi kusambazwa kama ulivyo  na ufuatiliaji wake ulifanyika ikabainika kuwa hazikuwa habari za kweli .

 Polisi wamebaini pia tukio lililoelezwa kuwa kuna mtu aliuawa Sinza kisha kuondolewa ziwa upande wa kushoto na sehemu za siri, hazikuwa habari za kweli na hakuna tukio la namna hiyo kama linavyoelezwa. Kuzusha taarifa za uongo zenye lengo la kujenga taharuki au hofu ni makosa.Tunatahadharisha juu ya tabia hizo na Jeshi halitasita kuwatafuta na kuwahoji wanaohusika kwa hatua zaidi za kisheria.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam pia katika kusimamia mifumo ya kisheria ya haki jinai limeendelea kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya kihalifu na hatimaye kupatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu. Jeshi la Polisi limekuwa likichukizwa sana na vitendo vya ubakaji na ulawiti na katika hatua hiyo mwaka 2023 Juni,  mshtakiwa Hussein Shomvi (50) fundi ujenzi, mkazi wa Chanika Zogoali alikamatwa na baadae kufikishwa Mahakama ya Kinyerezi  na baada ya mashauri yake kusikilizwa tarehe 10 Juni 2024 alipatikana na hatia ya kosa kulawiti watoto wawili wa kiume wa shule ya msingi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Washtakiwa wengine  Shamim Hamadi @dj mush (30) Mkazi wa Kimara Mwisho, na Waziri Ramadhani (26) Mkazi wa Mbezi Luis na Seif Salum (19) mkazi wa Manzese wote kwa pamoja mwaka 2022 walifikishwa Mahakama ya Kinondoni mbele ya Hakimu Mkazi Nabwike Mbaba na baada ya mashauri yao kusikilizwa terehe 10 Juni 2024 walipatikana na hatia ya Unyangayi wa kutumia silaha na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali, zitatunzwa na wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.