Jumatatu , 12th Aug , 2019

Boti inayomilikiwa na klabu ya starehe ya Yacht jijini Tanga, imepinduka baharini jana jioni Agosti 11, 2019, ikiwa na watu 11 wengi wao wakiwa ni wafanyakazi wa Benki ya NMB Korogwe.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Edward Bukombe.

Akiongea na EATV&EA Radio Digital, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Edward Bukombe, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

''Ni kweli ajali imetokea, na watu 10 waliokolewa na wakapata huduma ya kwanza hivyo wanaendelea vizuri. Mmoja hajapatika hadi sasa, jitihada za kumtafuta zinaendelea'', amesema Kamanda Bukombe.

Aidha Kamanda ameeleza kuwa watu hao walikuwa wamekuja kwaajili ya mapumziko ya sikukuu, hivyo wakawa wanataka kufika visiwa vya jirani na wakati wanakwenda ndio wakakumbwa na upepo mkali na walipotaka kugeuza ndio ikapinduka.

Kamanda ameongeza kuwa Boti hizo zinamilikiwa na klabu hiyo, hivyo hutoa huduma kwa wateja wao wanaotaka kufika visiwa vya karibu na eneo hilo, ambavyo haviko mbali na vinaonekana hata ukiwa mjini.