Jumatatu , 23rd Sep , 2024

Kada wa CHADEMA Boniface Jacob maarufu kama Boni Yai ataendelea kubaki mahabusu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushindwa kutoa uamuzi wa pingamizi la dhamana dhidi yake.

Kesi hiyo ilipangwa kutolewa uamuzi leo Septemba 23, 2024,mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga na ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 26,2024 baada ya Boni kutofikishwa mahakamani leo kwa sababu ambazo hazikutajwa.

Boni Yai nakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni ya kuchapishaji taarifa za uongo kwenye mitandao, kinyume cha sheria ya makosa ya mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Meya huyo wa zamani wa Ubungo Dar es Salaam, alipandishwa kizimbani mahakamani hapo Septemba 19, 2024, ambapo upande wa mashtaka pamoja na mambo mengine, uliiomba Mahakama izuie dhamana yake kwa madai ya usalama wake mshtakiwa, hoja zilizopingwa na jopo la mawakili wake likiongozwa na Peter Kibatala.