Jumanne , 4th Nov , 2014

Baraza la Wanawake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, nchini Tanzania limelaani vikali Vurugu alizofanyiwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba zilizotokea hivi karibuni.

Mwenyekiti wa BAWACHA, Mh. Halima Mdee akiwa na viongozi wengine wa Baraza hilo.

Akizungumza katika Mkutano wa Hadhara katika Ziara ya Baraza hilo kanda ya Ziwa Mwenyekiti wa BAWACHA, Mh. Halima Mdee amesema kitendo alichofanyiwa Jaji Warioba ambaye alishika Nyadhifa za Juu serikalini hakikubaliki.

Mh. Mdee amewaasa pia vijana wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam waepuke kujiingiza katika vurugu kama hizo ambazo zinahatarisha amani ya nchini na kusema wao kama chama watazunguka nchini nzima kuendelea kutoa elimu kuhusu kupinga Katiba Inayopendekezwa na Kujiandikisha ili kupiga kura katika Chaguzi za Serikali za Mitaa.

Nao Viongozi walioandama katika ziara hizo wamesema ni wakati wa wananchi sasa kukiondoa chama tawala madarakani kuanzia ngazi ya chini ya Serikali za Mitaa kwa kujiandikisha katika Daftari ili kufanya mabadiliko yatakayowaletea faida siku za mbeleni.