Aliko Dangote - Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote
Afisa Mtendaji Mkuu wa Dangote Tanzania, Bwana Harpreet Duggal amesema mafundi wa Dangote wapo kazini na shughuli za uzalishaji zitarejea katika siku chache zijazo.
Alisema kiwanda kilianza uzalishaji wa kibiashara mapema mwaka huu na kama ilivyo kwa kiwanda kingine kama hicho jambo lolote linaweza kutarajiwa hasa katika miezi ya mwanzo.
Hata hivyo alizitaja hitilafu hizo kuwa ni za kawaida na uzalishaji utarejea katika kipindi kifupi kijacho.
Alipoulizwa kuhusu gharama kubwa za uzalishaji, Bwana Duggal alisema unapolinganisha na gharama nyingine za uzalishaji katika Dangote, gharama za uendeshaji Tanzania ni za juu sana.
Alisema moja ya sababu kuu ni matumizi ya jenereta za dizeli katika kuendesha kiwanda na pia kiwanda kuwa mbali na soko kuu la saruji kumechangia ongezeko la gharama za usafirishaji.
Akasema serikali inaangalia suala hili la gharama na jinsi ya kutafuta njia ya kutupunguzia mzigo huu.
Akaongeza, “Tuna matumani makubwa kuhusu uwekezaji wetu wa muda mrefu hapa Tanzania na tupo makini, kwa kushirikiana na serikali tutaweza kuhimili gharama za uzalishaji ili tuweze kuendelea kufanya bidhaa ya saruji kuwa na bei nafuu nchini.”
Kiwanda cha Dangote kilichopo Mtwara chenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 600 kina uwekezaji mkubwa katika saruji kuliko vyote katika Afrika Mashariki. Kina uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na kutoa ajira ya moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1000 wa Mtwara.